Monday, August 5, 2013

WAFANYA BIASHARA WA MANISPAA YA SONGEA WATANGAZA MGOMO

 Hawa ni wafanya biashara wa masoko ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma wakiwa katika kikao 
-----------------------------------------------------------
Na Nathan Mtega,Songea


UMOJA  wa wafanyabiashara wa masoko ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma umeendelea kuulalamikia uongozi wa Manispaa ya Songea kwa kuongeza gharama za pango la vibanda na gharama za leseni za biashara kwa wafanyabiashra pamoja na utaratibu usioridhisha wa baadhi ya watumishi wa halmashauri hali hiyo imepelekea wafanyabiashara hao kuazimia kugoma.


Wakizungumza katika mkutano wa dharula wanachama zaidi ya themanini wa umoja huo wamesema hawakubaliani na utaratibu wa uendeshaji wa masoko yaliyopo ndani ya manispaa hiyo ikiwa ni pamoja na ogezeko la pango lililoamriwa na uongozi wa manispaa bila kuwashirikisha wafanyabiashara hao.


Wamesema uwezo wa wafanyabiashara katika masoko ya Manispaa ya songea na mzunguko wa fedha uliopo hauendani na ongezeko hilo la kodi,ushuru na utaratibu wa kuwataka wafanyabiashara hao  kuomba tenda ya kuendelea kufanya biashara katika vibanda hivyo walivyokuwa wakifanyia biashara zao.


Wakizungumza wafanyabiashara Christian Kayombo na Hamis Machaku katika mkutano huo wamesema kuwa utaratibu unaofanywa na uongozi wa Manispaa wa kuongeza pango la vibanda na kutangaza tenda kwa ajili ya vibanda hivyo ambavyo wao wamekuwa wakivitumia kwa mkataba wa muda  mrefu bila kushirikishwa kwenye maamuzi hayo mapya ni ishara ya unyanyasaji kwao na hawajatendewa haki kwa sababu walishaomba kupunguzwa kwa kodi pamoja na malipo ya leseni lakini kabla maombi hayo hayajafanyiwa kazi wanaletewa ongezeko la kodi.


 Wamesema kuwa ni vyema uongozi wa Manispaa ukaona umuhimu wa kuwashirikisha wafanyabiashara kwa kupitia viongozi wa umoja wao katika kutoa na kufikia maamuzi yanayowahusu badala ya uongozi huo kukaa na kuamua juu ya wafanyabiashara wakati ukijua hali za biashara katika Manispaa ya Songea na mzunguko wa fedha ulivyo.


Aidha wafanyabiashara hao wametangaza kugoma siku ya Jumanne 6 Agosti 2013  kwa muda usiojulikana kuendesha biashara ikiwa malalamiko hayo hayatafanyiwa kazi kwa sababu kumekuwepo na vitendo vingi vya unyanyasaji vinavyofanywa na baadhi ya watumishi wa halmashauri dhidi ya wafanyabiashara na hususani wafanyabiashara wadogo .


Akizungumza makamu mwenyekiti wa umoja wa wafanyabiashara wa masoko ya Manispaa ya Songea Leornad Chiwangu alisema wafanyabiashara wameazimia kuanza mgomo huo siku ya Jumanne na utaendelea kwa muda usiojulikana ikiwa malalamiko na maombi yao hayatafanyiwa kazi.

Habari kwa hisani ya www.demashonews.blogspot.com

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...