TAARIFA YA ZITTO ZUBERI KABWE (MB) KUHUSU
KUVULIWA NAFASI ZA
UONGOZI NDANI YA CHAMA CHANGU CHA CHADEMA
1. Utangulizi
i. Katika kikao chake cha siku mbili kilichofanyika tarehe 20 22
Novemba 2013 ,
Kamati Kuu ya CHADEMA, pamoja na mambo mengine, iliazimia kunivua
nafasi zangu zote za uongozi ndani ya chama. Kwa mujibu wa taarifa ya
chama
iliyotolewa katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Ijumaa
tarehe 22
Novemba 2013, ilielezwa kwamba sababu za kuvuliwa uongozi mimi na Dk
Kitila Mkumbo ni uhaini na hujuma kwa chama kutokana na waraka
unaojulikana
kama mkakati wa uchaguzi 2013.
Ukweli ni kwamba waraka uliotajwa si
sababu
ya mimi kuvuliwa nafasi zangu za uongozi kama ilivyojadiliwa katika
Kikao cha
Kamati Kuu . Sababu za kufukuzwa kwangu kama zilizojadiliwa katika
kikao cha
Kamati Kuu ni tuhuma lukuki ambazo si mara yangu ya kwanza kuzisikia
zikijadiliwa ndani na nje ya vikao vya chama. Hitimisho la tuhuma hizi
ni kwamba
mimi nimekuwa nikikisaliti chama kwa kutumika na CCM na Usalama wa
Taifa.
Nitazianisha tuhuma hizi na kuzijibu kama ambavyo nimekuwa nikizijibu
katika
vikao mbalimbali vyama.
ii. Ninatambua
kwamba chama changu kinapita katika wakati mgumu sana sasa
hivi. Nataka nitamke mapema sana kwamba mimi Zitto Zuberi Kabwe
sitokuwa
chanzo cha CHADEMA kuvunjika. Hiki ndicho chama kilichonilea na
kunifikisha
hivi nilivyo. Ningependa chama hiki mtoto wangu atakapokuwa mtu mzima
na
atakapoamua kujiunga na siasa aingie CHADEMA. Bado nina imani kubwa na
chama changu na ninaamini
ndicho kinachostahili kuendesha nchi jana,
leo na kesho.
2. Kuhusu tuhuma mbalimbali zinazo elekezwa
kwangu
Zipo tuhuma nyingi ambazo zimekuwa zikirudiwarudiwa katika vikao vya
chama na
nje ya vikao na baadhi ya viongozi wenzangu. Tuhuma hizi zinalenga
kuonyesha
kwamba mimi ni mbinafsi na kwamba ninapokea rushwa ili kukihujumu
chama
changu. Nitazianisha tuhuma kwa kifupi na kuzijibu kama ambavyo
nimekuwa
2
nikizijibu katika vikao mbalimbali vya chama.
i) Tuhuma kwamba sikushiriki kumpigia kampeni mgombea wetu wa urais
katik a
uchaguzi wa mwaka 2010. Ningependa kueleza yafuatayo kuhusu jambo
hili:
●
Mimi nilikuwa mgombea wa ubunge katika Jimbo la Kaskazini huko Kigoma.
●
Pamoja na kuwa mgombea wa ubunge, nilifanya kampeni katika majimbo mengine
16 katika mikoa mbalimbali, ikiwemo Dar es Salaam, Mtwara, Pwani,
Shinyanga,
Mara na Rukwa. Hakuna kiongozi yeyote wa juu aliyefanya kampeni katika
majimbo
mengi kama mimi, ukiacha mgombea urais.
●
Kote nilipopita nilimpigia kampeni wagombea wetu wa udiwani, ubunge na Rais.
●
Katika Mkoa wa Kigoma nilizunguka na mgombea urais katika kata zote za Kigoma
Kaskazini na majimbo yote manane ya Mkoa wa Kigoma.
ii) Tuhuma kwamba katika Mkoa wa Kigoma nilishindwa kuwapigia kampeni
wagombea wetu kiasi kwamba peke yangu ndiye niliyeshinda katika
uchaguzi huo.
Ukweli ni kwamba niliwapigia sana kampeni wagombea wetu, na hivyo
ndivyo wapiga
kura wa Kigoma walivyoamua.
iii) Tuhuma kwamba nilishiriki kuwashawishi wagombea wetu katika
baadhi ya
majimbo kujitoa katika uchaguzi wa mwaka 2010 ili kuwapisha wagombea
wa CCM
wapite bila kupingwa kwa njia ya rushwa. Majimbo yanayotajwa ni pamoja
na
Sumbawanga, Musoma Vijijini na Singida Mjini. Kama nilivyokwisha
kueleza katika
vikao mbalimbali vya chama jambo hili si la kweli na hakuna popote ambapo
watoa
tuhuma hizi wamewahi kutoa ushahidi kwamba nilifanya jambo hili. Nipo
tayari kwa
uchunguzi ndani ya chama na watoa tuhuma waje na ushahidi bayana wa
jambo hili. Si
afya kwa chama kuendelea kurudiarudia tuhuma hizi kila mara tangu
mwaka 2010 bila
uchunguzi wowote kufanyika na jambo hili lifikie mwisho.
iv) Tuhuma kwamba nimekuwa sishiriki katika operesheni mbalimbali za
chama: Ukweli
ni kwamba nimeshiriki sana katika operesheni mbalimbali za chama ndani
na nje ya
nchi. Kwa mfano, mwaka 2011 tulikuwa na operesheni kubwa katika mikoa
ya Kanda
ya Nyanda za Juu Kusini na nilikwenda katika mikoa yote
tuliyotembelea. Mwaka 2012
3
baada ya hoja ya mkonge bungeni nilifanya ziara Mkoa wa Tanga. Mwaka
201 2
kulikuwa na operesheni kubwa moja katika mikoa ya kusini ya Mtwara na
Lindi.
Operesheni hii sikushiriki kwa sababu nilikuwa nchini Marekani
kufungua matawi kwa
mwaliko wa Watanzania wanaoishi huko.
v) Tuhuma kwamba
nimekidhalilisha chama kwa tamko la PAC kwamba Hesabu
za Vyama hazijakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG): Katika jambo hili ninatuhumiwa kwamba
mimi kama Naibu Katibu
nilipaswa kuwasiliana kwanza na viongozi wa chama 'kuwatonya' ili wajiandae.
Kwamba kutokuwatonya kumekidhalilisha chama na kukiweka kundi moja na
CCM na
nastahili kuadhibiwa vikali kwa kuwa katika taarifa yangu nilikuwa na
nia mbaya na
chama chetu. Maelezo yangu niliyoyatoa na ambayo ningependa kuyakariri
hapa
kuhusu jambo hili ni kama ifuatavyo:
●
Utawala bora hautaki mimi kutumia nafasi yangu ya uenyekiti wa PAC kulinda
chama changu na kuonea vyama vingine. Kufanya hivyo ni kuendeleza
tabia zile zile
ambazo tunazipinga na ambazo tunapigania kuzibadilisha
●
Napenda kusisitiza kwamba hakuna chama ambacho kimewahi kukaguliwa na
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG). Natambua kwamba mahesabu
ya
chama changu yamekuwa yakikaguliwa na wakaguzi wa nje kwa utaratibu
tuliojiwekea. Lakini matakwa ya kisheria ni kwamba mahesabu ya vyama
vya siasa
hayajakaguliwa na CAG, na hili ni kosa la kisheria, bila kujali kosa
hili ni la nani.
vi) Tuhuma kwamba mimi ni mnafiki katika kukataa
kwangu kuchukua Posho
za Vikao
Mtakumbuka kwamba mimi nilikataa kuchukua posho tangu mwaka 2011 kama
ishara
ya kuonyesha kwa vitendo msimamo wa chama chetu wa kupinga posho za
kukaa na
matumizi mengine yasiyofaa katika fedha za umma kama ilivyoanishwa
kwenye Ilani
yetu ya mwaka 20102015.
Mtakumbuka kwamba hivi karibuni Mheshimiwa Lema
amenishutumu kwamba kukataa kwangu kuchukua posho ni unafiki kwa
sababu
ninapokea posho kubwa zaidi katika mashirika ya umma ambapo mimi ni
mwenyekiti
wa kamati husika. Ninapenda kueleza yafuatayo kuhusu jambo hili:
●
Sipokei posho yeyote ya vikao (sitting allowance) ndani na nje ya Bunge tangu
4
mwaka 2011. Hii ni pamoja na vikao vyote katika Kamati za Bung e
ninavyohudhuria. Mtu yeyote mwenye ushahidi vinginevyo auweke
hadharani.
●
Swala la kukataa posho (sitting allowance) ni swala la kiilani katika chama
chetu, na
kwangu ni swala la kimisingi
zaidi. Katika Wilaya yangu vifo vya kina
mama
wajawazito ni 1900 kati ya wanawake 100,000 wenye ujauzito.
Vifo hivi
vinatokana
na ukosefu wa huduma kwa sababu ya bajeti finyu. Ndiyo maana
nilifurahi sana kwa
chama chetu kuliweka swala la kupunguza matumizi ya Serikali katika
Ilani, na
kuondoa posho za wabunge, ambao tayari wanapokea mishahara mikubwa,
kungesaidia sana kupatikana fedha ambazo zingeokoa vifo vingi vya kina
mama.
● Jambo hili si suala la ugomvi baina yangu na
Mheshimiwa Lema. Ni suala la
msingi katika chama chetu.
3.
Usambazaji wa Ripoti ya Siri kuhusu
Zitto Kabwe
Hivi karibuni kulisambazwa waraka unaoitwa ripoti ya siri kuhusu mimi
ukibeba lundo la
tuhuma kwamba nimehongwa fedha nyingi ili kukihujumu chama changu.
Waraka huu
ulidaiwa kuwa umechomolewa kutoka makao makuu ya CHADEMA. Jambo hili
pia
lilijadiliwa katika kikao cha juzi kwa kifupi, na majibu ya viongozi
wa chama ilikuwa ni
kwamba waraka huu haukuandaliwa wala kusambazwa na makao makuu. Katika
mchango wangu nililalamikia mambo matatu yafuatayo:
i. Kwamba baadhi ya waliokuwa wanasambaza waraka ule walikuwa ni
viongozi wa
chama chetu. Bahati mbaya hadi leo hakuna hata mmoja ambaye
amekwishachukuliwa hatua za kinidhamu. Ninaamini kwamba kuna siku watu
hao
watachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu za chama chetu.
ii. Kwa kuwa chama kimekana rasmi kuhusika na waraka huu, nitaendelea
na taratibu
za kisheria ili kuhakikisha kwamba wote waliohusika kutengeneza hekaya
ile
wanachukuliwa hatua stahiki za kisheria.
4. Hitimisho
a) Ninatambua kwamba kuna watu walitegemea leo ningejibu mapigo na
ningewazodoa watu kwa majina kama ilivyo kawaida katika siasa za
Tanzania.
Natambua pia kwamba, kama ilivyo kawaida wakati wa migogoro katika
vyama vya
5
siasa hapa Tanzania, kuna watu walitegemea leo ningetangaza 'maamuzi
magumu' .
Natambua kwamba wapo ambao wangependa kupata
nafasi ya kuendelea
kutumia suala hili katika harakati zao za
kudhoofisha mapambano ya
demokrasia na uthabiti wa siasa za ushindani
nchini mwetu. Napenda
wanachama wa CHADEMA na wapenda demokrasia na siasa safi wote nchini
watambue kwamba mimi bado ni mwanachama mwaminifu wa chama hiki na
nitakuwa wa mwisho kutoka kwenye chama hiki kwa hiari yangu. Nitafuata
taratibu
zote ndani ya chama katika kuhitimisha jambo hili.
b) Naomba wanachama waelewe kwamba mimi kama binadamu ninaumia
ninapopigwa. Tuhuma ninazorushiwa ni kubwa na zinanikwaza. Tuache
siasa za
uzushi ili tujenge chama chetu na nchi yetu, ili hatimaye tuwakomboe
Watanzania
wenye matarajio na imani kubwa kwa chama chetu.
c) Kama mwanasiasa kijana niliyekaa katika siasa
kwa muda sasa yapo mengi
mazuri nimeyafanya. Lakini kuna maeneo
nilipojikwaa na yapo makosa
niliyofanya kisiasa katika maisha yangu ya
siasa.
d) Kinachoendelea ndani ya chama chetu ni mapambano ya kukuza
demokrasia. Ni
mapambano baina ya wapenda demokrasia dhidi ya wahafidhina, waumini wa
uwajibikaji dhidi ya wabadhirifu na wapenda siasa safi dhidi ya
watukuzao siasa
majitaka. Hii ni changamoto kubwa ndani ya chama chetu inayohitaji
uongozi
shupavu kuikabili. Nitasimama daima upande wa demokrasia. Kama
alivyopata
kunena mmoja ya wanasiasa maarufu, 'kiwango cha juu kabisa cha
uzalendo katika
nchi ni kukubali kutofautiana kimawazo', na ninatamani huu ndio uwe
utamaduni wa
chama chetu.
Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Dar es Salaam.
24 Novemba, 2013
|