Wednesday, August 14, 2013

RUVUMA: KILIMO CHA TUMBAKU CHA ZIDI KUSHUKA

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgfWi5cfhtpGsy9EqI9qmtDSsEavGIAUYejzSu-sd1rRjtcExDkXMkgvKKnPlrOns0kqZhK1P_NpxoyiChKxEu39bkr2nwY-kI06zGRcaNf0OoV1I3q3kCNlzWRpqjyT8_iHqJHzjy94SI/s640/tumbaku+nomba+moja.JPG 
Hili ni zao la tumbaku linalimwa Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma (Picha na Maktaba)
-------------------------------------------------
Na Fulmence Mbunda wa Demashonews NAMTUMBO.

IMEELEZWA kuwa kushuka kwa uzalishaji wa zao la tumbaku wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma kumesababishwa kwa kiasi kikubwa na kuwepo kwa viongozi  wezi na wasiokuwa na huruma kwa wakulima hivyo kama hawatashughulikiwa huenda jitihada za wakulima hao za kujikwamua kiuchumi zikashindwa kufikiwa.

Hali hiyo imepelekea wakulima katika maeneo mengi ya wilaya hiyo kuvunjika moyo na  matokeo yake kaya zinazojihusisha na kilimo hicho kumepungua kutoka kaya 12,000 hadi kufikia kaya 6600 huku kiasi cha tani zinazozalishwa nazo  kupungua kwa kiwango kikubwa kutoka  tani 350 milioni hadi kufikia  kilo 2,900,000 na ndiyo iliyosababisha uchumi wa wilaya kupungua kutokana na kushuka kwa uzalishaji wa zao hilo kwa kipindi cha miaka mitatu sasa.

Hayo yalisemwa na mkuu wa wilaya hiyo Abdula Lutavi hivi karibuni wakati alipokuwa akiongea na waandishi wa habari juu ya hatua aliyoichukua kukabiliana na wizi unaofanywa na viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika katika wilaya yake.

“kuna tatizo kubwa katika vyama vya msingi vya ushirika,hapa kuna wizi mkubwa unaofanywa na viongozi hao dhidi ya wakulima wetu ndiyo maana wakulima sasa hawataki  kusikia tena kilimo cha tumbaku na yote haya yamesababishwa na viongozi wasiokuwa na aibu”alisema Lutavi.

 Alisema kuwa viongozi  katika vyama vingi vya ushirika vilivyopo katika wilaya ya Namtumbo wamekuwa na tabia mbaya ya  kuwakata makato makubwa wakulima hali iliyowasababishia wakulima wa tumbaku maumivu makubwa na kwamba vitendo hivyo vichafu vimepelekea wakulima wazalishaji wakate tamaa ya kuongeza uzalishaji wa zao hilo.

 Aidha Lutavi amekinyooshea kidole chama kikuu cha ushirika cha wilaya ya Songea na Namtumbo(SONAMCU)kutokana na kufanya hujuma dhidi ya wakulima wa tumbaku kwa kuchukua mikopo kutoka katika taasisi za fedha na mzigo huo kuwaachia  wakulima tena kwa kuongeza kiasi kikubwa cha fedha tofauti  na zile zilizopitishwa kwenye vikao halali vya wanachama  wote.

 Katika hatua nyingine mkuu huyo wa wilaya amewaagiza viongozi wa  vyama vya ushirika katika wilaya hiyo  kurudisha fedha zote walizowakata wakulima bila utaratibu na kwamba kama hawatatekeleza hilo watachukuliwa hatua kwani wamekwenda kinyume cha sheria huku wakijinufaisha wao na kuwaacha wakulima wakiwa  na hali  ngumu ya maisha.

                  Habari kwa hisani ya demashonews.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...