Akizungumza na MTANZANIA Jumatano kwa
sharti la kutotajwa jina, mmoja wa askari aliyepo ndani ya kikosi cha
JWTZ huko nchini Kongo, alisema maofisa hao wanashikiliwa kwa mahojiano
zaidi.
Taarifa hizi za sasa zinakuja wakati
ambapo kumekuwa na madai ya muda mrefu, ambayo yamekuwa yakitolewa na
Umoja wa Mataifa pamoja na Marekani kwamba, Rwanda imekuwa ikiwasaidia
waasi wa kundi la M-23.
Pamoja na kwamba Rwanda imekuwa ikipinga
madai hayo, kitendo chake cha wiki iliyopita cha kuamua kupeleka
bataliani mbili zenye wanajeshi 1,700 ili kukabiliana na kile
kinachodaiwa kuwa ni kishindo cha vikosi vya Umoja wa Mataifa vyenye
jukumu la kulinda amani katika taifa hilo lenye utajiri mkubwa
kirasilimali, kinatokana na waasi wa M23 kupata kipigo kikali.
Chanzo chetu hicho kutoka uwanja wa
mapambano nchini Kongo, kililidokeza gazeti hili kuwa maofisa hao wa
Jeshi la Rwanda waliwakamata katika mapigano hayo yaliyodumu kwa zaidi
ya wiki moja, ambayo tayari yamewakimbiza waasi wa M23.
“Askari wa Rwanda tuliowakamata, ni
maofisa wa ngazi za juu kabisa jeshini, tena walikuwa na sare za jeshi
hilo… walikuwa wakiwasaidia hao M23, lakini kwa kuwa sisi tulikuwa
makini tulifanikiwa kuwatandika hadi tukawakamata,” kilisema chanzo
chetu hicho.
Habari za uhakika kutoka vyanzo vya
habari vya kuaminika zinaeleza kwamba, hatua hiyo ya kuwakamata maofisa
hao pamoja na kuondoka kwa waasi wa kikundi cha M23, imefanikisha
kushinda vita hiyo kwa zaidi ya asilimia 95.
Mtoa taarifa wetu huyo kutoka Kongo,
ameliambia gazeti hili kuwa, tayari Monusco wanaoongozwa na JWTZ
wameanza kufurahia ushindi huo na kwamba sasa hivi wanasubiri tamko
kutoka kwa wakuu wao, ili kufahamu kinachofuata baada ya kufanikisha
hatua hiyo.
MAPIGANO YALIVYOKUWA
Akielezea namna walivyofanikiwa kutoa
kibano kwa M23, askari huyo kwanza alikiri kuwa mapigano yalikuwa
makali, kutokana na kikundi hicho cha waasi kusheheni vifaa vya kisasa
na msaada wanaoupata kutoka Serikali ya Rwanda.
“Kwa kweli mapigano yalikuwa makali
sana, lakini kwa upande wetu sisi tulikuwa tunajiamini kutokana na vifaa
ambavyo pia ni vya kisasa hususani ikizingatiwa jeshi letu ni la Umoja
wa Mataifa.
“Tulifanikiwa kuteka ngome yao kwa kutumia mbinu mbalimbali za kijeshi na kuwafanya watawanyike kabisa katika eneo hilo.
“Ngome yao ilikuwa ni kubwa sana, ina
ukubwa wa zaidi ya viwanja vitatu vya mpira… na katika eneo hilo
kulikuwa kumesheheni vifaa vyao vya kivita, kama makombora, mafuta,
mizinga pamoja na vifaa vingine kama magari na baadhi ya silaha nyingine
kubwa kubwa za kivita,” alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo, sasa hali ni shwari ndani ya nchi hiyo ya Kongo.
“Baada ya kuwasambaratisha sasa
wamekimbilia eneo moja lililopo karibu na mpaka wa Uganda. Kama
unavyofahamu hawa jamaa walikuwa wakitumia mbinu za kujihami kwa kurusha
mabomu katika eneo la Rwanda, ili ionekane kuwa sisi tumerusha,”
alisema askari huyo.
“Lakini tunamshukuru Mungu, tupo salama
ingawa tumempoteza askari mmoja na askari wengine wenzetu wa Tanzania
ambao ni wanne, wamepata majeraha kidogo lakini wanaendelea vizuri.
“Hivyo nawaomba Watanzania wenzangu
waendelee kutuombea turudi salama, kwa sababu kazi sasa imeshakamilika,”
alisema askari huyo.
Juhudi za gazeti hili kumpata msemaji wa Monusco, Luteni Kanali Prosper Basse kuzungumzia juu ya taarifa hizo, zilishindikana.
Taarifa ambazo tumezinasa kwa siku
kadhaa sasa kutoka uwanja wa mapambano na ambazo zimegusa vichwa kadhaa
vya habari zinaeleza kuwa, brigedia maalumu ya vikosi vya UN yenye
dhamana ya kujibu mashambulizi (FIB), katikati ya wiki iliyopita
iliendesha operesheni kubwa iliyoharibu kabisa ngome muhimu ya waasi wa
M23, hali inayotajwa na wachambuzi wa mambo kuwa ndiyo iliyoishtua
Serikali ya Rwanda ambayo inatuhumiwa kuwasaidia waasi hao.
Taarifa za kijeshi zinaeleza kuwa, FIB
ambayo inaundwa na wanajeshi wapatao 3,000 kutoka Tanzania na Afrika
Kusini chini ya Azimio Namba 2098 la Baraza la Usalama la Umoja wa
Mataifa, limejizatiti kwa zana za kisasa za kivita zikiwamo mizinga na
helikopta za kivita.
Taarifa kutoka mashariki ya Kongo
zinaeleza kwamba, mashambulizi dhidi ya waasi wa M23 ambao hivi karibuni
waliripotiwa kusababisha kifo cha mwanajeshi mmoja wa Tanzania aliye
katika jeshi la UN, yamesababisha waasi hao kukimbilia katika eneo la
milima lililopo umbali wa kilomita tano kutoka mji mdogo wa
Kanyaruchinya Mashariki mwa Goma.
M23 WAZUNGUMZA
MTANZANIA Jumatano jana lilifanikiwa
kuzungumza na Rais wa M23, Bertrand Bisiimwa, ambapo pamoja na mambo
mengine alieleza sababu za vikosi vyao kuondoka katika ngome yao ya
kivita sambamba na taarifa za kuibuka kwa mapigano mapya ya hivi
karibuni.
Katika hilo, Bisiimwa alikiri kikosi
chake kurudi nyuma siku nne zilizopita, huku akiitaja sababu ya kufanya
hivyo kuwa ilitokana na wao kutotaka vita baada ya majeshi ya Kongo
kuanza kuwarushia mabomu kwenye kambi yao.
“Sisi tuliamua kurudi nyuma tusiendeshe
vita, tunajua aliyetupa hayo mabomu ambayo yalifika mpaka Rwanda,
tunaitaka Umoja ya Mataifa ikuje ifanye uchunguzi wake…wakuje waangalie
vifaa yetu waone kama inaweza kurusha mabomu hadi Rwanda,” alisema.
Hata hivyo, Bisiimwa alisema kuwa sio
kweli kama majeshi ya Umoja wa Mataifa yakiongozwa na JWTZ
yaliwasambaratisha katika ngome yao.
“Sio kweli walikuja Kanyaruchina tukiwa
tumeondoka na tuliondoka si kwa sababu ya kuwakimbia, hapana tulitaka UN
wafanye uchunguzi yake juu ya kurushwa mabomu, kwa sababu wanataka
kutuvalisha mambo ya uongo mchafu,” alisema Bisiimwa.
Bisiimwa alijigamba kuwa majeshi ya
Kongo hayawawezi na kwamba walikwishawashindwa, lakini akakiri kwamba
majeshi ya Umoja wa Mataifa wanaweza kuwaondoa.
“Ninakiri hiyo kwa sababu Umoja wa
Mataifa inaweza kututoa, unajua inakuwa na nguvu ya hatari,” alisema
Bisiimwa kwa Kiswahili cha tabu.
CHANZO-Mtanzania
No comments:
Post a Comment