MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam
imetupilia mbali pingamizi la Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), na
kuzikubalia kampuni tano za simu nchini kujiunga katika kesi ya kupinga
tozo ya kodi za simu ya Sh 1,000 kwa kila laini kwa mwezi. Kampuni hizo
zinaungana na Chama cha Kutetea Walaji kupinga utekelezaji wa kodi hizo
uliotakiwa kuanza Julai mwaka huu, baada ya kupitishwa bungeni Juni
mwaka huu.
Akitoa uamuzi wa jopo, Mwenyekiti wa
Jopo la majaji, Jaji Aloysius Mujuluzi, alisema wamekubaliana na hoja
zilizowasilishwa na wakili wa kampuni tano za simu, Fatuma Karume,
kwamba hati ya kiapo iliyowasilishwa mahakamani na wateja wake iko
sahihi.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali
akimwakilisha AG aliwasilisha pingamizi la awali kupinga maombi ya
kampuni za simu kujiunga katika kesi akidai kwamba, hati ya kiapo
ilikosewa kisheria kwani aliyeapa ni mmoja, Tumaini Shija wa Kampuni ya
TTCL.
“Tunakubaliana na hoja za Karume
kwamba hoja za kupinga maombi ya kampuni za simu kujiunga katika kesi
hayana msingi, kwa sababu sheria ina ruhusu mtu kuapa kwa niaba ya
wengine.
“Kampuni tano za simu, MIC Tanzania
Limited, Vodacom, Airtel, ZANTEL na TTCL zimekubaliwa kuingia katika
kesi, watakuwa mlalamikaji namba mbili mpaka sita, mlalamikaji namba
moja ni Chama cha Kutetea Walaji,” alisema Jaji Mujuluzi.
Jaji Mujuluzi alisema walalamikaji
hao baada ya kuungana watafanya marekebisho ya hati ya maombi yao, na
Oktoba 15 mwaka huu wataiwasilisha mahakamani, Jamhuri itawasilisha
majibu, kisha Oktoba 21 maombi ya kupinga tozo za simu yatasikilizwa.
Mdaiwa katika kesi hiyo ni Wizara ya Fedha na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Chama cha Walaji kiliwasilisha maombi
mahakamani dhidi Wizara ya Fedha hivi karibuni wakipinga tozo hiyo kwa
madai kwamba inawaumiza wateja wao.
Wakili Karume akiziwakilisha kampuni
za simu, aliwasilisha maombi mahakamani wakitaka waruhisiwe kujiunga
katika kesi hiyo na wamekubaliwa.
Majaji wanaosikiliza kesi hiyo ni
majaji watatu, Aloysius Mujuluzi (Mwenyekiti wa jopo), Jaji Laurence
Kaduli na Jaji Salvatory Bongole.
Walalamikaji hao sita wamewasilisha maombi mahakamani hapo wakipinga sheria mbalimbali zinazokiuka Katiba.
Wanadai wateja wao hawana uwezo wa
kulipa kodi ya Sh 1000 kwa kila laini ya simu iliyopitishwa bungeni Juni
mwaka huu, hivyo wanaitaka Mahakama kuzuia utekelezaji wa kutoza kodi.
No comments:
Post a Comment