Friday, April 12, 2013

WANAHABARI WAWILI NA AFISA UHAMIAJI WAPOTEZA MAISHA KATIKA AJALI YA GARI HANDENI

MAREHEM HUSSEIN SEMDOE MWANDISHI WA GAZETI LA MWANANCHI ALIYEFARIKI KWENYE AJALI
WAANDISHI wa habari wawili pamoja na Ofisa Uhamiaji wa Wilaya ya Handeni wamefariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea leo majira ya saa nne asubuhi nje kidogo ya Mji wa Handeni. Waliofariki dunia ni Hussein Semdoe  mwandishi wa gazeti la Mwananchi, Hamis Bwanga wa Radio Uhuru na Abood pamoja na Mariam Hassan ambaye ni Ofisa Uhamiaji Wilaya ya Handeni.

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo pamoja na vifo vya marehemu hao. Mkuu  huyo wa Wilaya hiyo amesema ajali hiyo imetokea wakiwa kwenye msafara kuelekea Ndolwa kupanda miti.

Akifafanua zaidi juu ya ajali hiyo, Muhingo alisema gari lililopata ajali ni la Mkurugenzi wa Halmashauri ya Handeni, STJ 4673 ambalo ndilo lililokuwa likitumiwa na Ofisa Uhamiaji, Hassan pamoja na wanahabari hao.
Akizungumzia mazingira ya ajali alisema ajali imetokea baada ya gari hilo kupasuka tairi la nyuma likiwa kwenye mwendo kisha kupoteza uelekeo na kuanguka. “Baada ya kupoteza uelekeo lili binuka kando ya barabara na marehemu wote walitupwa nje ya gari na kuangukia mawe hivyo kupoteza maisha, wawili walifia papo hapo na mmoja baadaye,” alisema Muhingo.

Alisema dereva pekee ndiye aliyenusurika katika ajali hiyo na amelazwa kwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya Handeni. “…Dereva naye alirushwa nje wakati wa ajali pamoja na marehemu wote, lakini yeye aliangukia juu ya kichaka hivyo kutoumia sana,” alisem kama wenzake.

Alisema msiba huo ni mkubwa kwa Wilaya ya Handeni kwani wamepoteza wachapakazi na watu muhimu katika mchakato wa maendeleo ya wilaya hiyo. Aliongeza kuwa Wilaya ya Handeni imepoteza wanahabari kwa asilimia 100, kwani waandishi hao ndiyo waliokuwa wanahabari pekee wilayani hapo. “…Msiba huu ni mkubwa si kwa tasnia ya wanahabari pekee bali hata kwa juhudi za maendeleo ya Wilaya ya Handeni, tulikuwa tukizunguka nao katika shughuli mbalimbali hapa Wilayani hivyo ni pigo kubwa,” alisema muhingo.
Aliongeza kwa upande wa Ofisa Uhamiaji, marehemu Hassan alikuwa ni mpambanaji mkubwa wa wahamiaji
haramu katika wilaya Hiyo, na hivi karibuni alifanikiwa kuwakamata takribani wahamiaji 70 eneo hilo, hivyo kifo chake ni pigo kubwa kwa nguvu kazi ya wilaya. Alisema tayari miili ya marehemu wawili (Mdoe na Hassan) imechukuliwa kwa shughuli za mazishi na mmoja bado (Bwanga) unasubiri wanandugu kutoka Handeni.(HABARI NA PICHA KWA HISANI YA THE HABARI.COM)

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...