Sunday, May 26, 2013

VIKONGWE WATATU WAUAWA KIKATILI BUNDA MKOANI MARA



MATUKIO KAMA  HAYA YAMEZIDI KUFUMMBIWA MACHO NA YANAZIDI KUTOKEA KAMA WALIVYOUAWA KIKATILI  VIKONGWE WATATU HUKO BUNDA MKOANI MARA
WANAWAKE watatu wameuawa kikatili kwa kukatwa mapanga na wananchi wanaojiita wenye hasira na kisha miili yao kuteketezwa kwa moto, wilayani Bunda mkoani Mara.
Kamanda wa Polisi Kamishina Msaidizi wa Polisi, Absalom Mwakyoma alisema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia jana katika vijiji vya Nyamitwebi na Kasahunga, wilayani hapa.
Aliwataja watu waliouawa kuwa ni Tibezuka Biseko au Bibi Rai (51), mkazi wa Kijiji cha Nyamitwebili, Chausiku Rubisha (73) na Mugara Manyama (75) wakazi wa Kijiji cha Kasahunga.
Alisema wanawake hao waliuawa na wananchi waliopiga yowe wakiwatuhumu kuwa ni wachawi, huku wakidai kuwa walimchukua kichawi ndugu yao mmoja aliyefariki dunia hivi karibuni katika ajali ya gari baada ya kugongwa akiwa anaendesha pikipiki.
Aidha, alisema kuwa pia wananchi hao waliziteketeza kwa moto nyumba tano za wanawake hao pamoja na nyumba nyingine za wanawake wengine ambao walinusurika kuuawa baada ya kupata taarifa na kutoroka.
“Wanawake watatu wameuawa katika tukio hilo na nyumba zao zimeteketezwa kwa moto… na hili tukio linahusishwa na imani za ushirikina, baada ya kuambiwa na waganga wa jadi.
“Hawa waganga feki wanawatia hasira wananchi kwa mambo ya kijinga kiasi hiki, hatuwezi watu kuwa tunauawa kinyama, maana hawa wazee walitakiwa waishi kama watu wengine,” alisema.
Akifafanua juu ya tukio hilo, Kamanda Mwakyoma alisema kuwa hivi karibuni mwanaume mmoja aitwaye Phales Wegero, aligongwa na gari wakati akiendesha pikipiki hali iliyosababisha wananchi wenye hasira kuiteketeza kwa moto gari hiyo.
Alisema baada ya mwanaume huyo kugongwa, ndugu zao walipiga ramli kwa waganga wa jadi na kuambiwa kuwa amechukuliwa kichawi, na kwamba wachawi hao wamekuwa wakimtembeza usiku kijijini hapo.
Kamanda Mwakyoma alisema kuwa hali hiyo iliwafanya wananchi hao kujikusanya baada ya kupiga yowe na kuwavamia wanawake hao kwa nyakati na maeneo tofauti na kuwashambulia hadi kuwaua.
Aliongeza kuwa pia wauaji hao wameviteketeza kwa moto vitu vyote vya watu hao, zikiwemo thamani za ndani.
Alisema kuwa kuhusiana na tukio hilo la jana, wanawashikilia watu kadhaa kwa mahojiano zaidi na upelelezi wa tukio hilo bado unaendelea, ikiwa ni pamoja na kuwasaka wengine wanaodaiwa kutoroka.
Kutokana na tukio hilo, baadhi ya wananchi wameyakimbia makazi yao na kukimbilia milimani wakiogopa kukamatwa na polisi.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...