Wednesday, July 24, 2013

MMILIKI WA HOME SHOPPING CENTRE APELEKWA AFRIKA KUSINI

picha hii ni ya sheha wa shehia ya tomondo wilaya ya magharibi unguja Mohammed Omar Said,alipomwagiwa tindikali huko Zanzibar,Tukio kama hili limemkuta mmiliki wa maduka ya Home Shopping Centre bw Said Mohammed Saad
MFANYABIASHARA maarufu na Mmiliki wa maduka ya Home Shopping Center(HSC), Said Mohamed Saad, ambaye wiki iliyopita alimwagiwa tindikali maeneo ya Msasani City Mall, jijini Dar es Salaam, amepelekwa Afrika Kusini kwa matibabu zaidi. Taarifa zilizopatikana Jumatano na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camilius Wambura, zinaeleza kuwa alipelekwa Afrika Kusini juzi.

Kamanda Wambura alisema ni kweli kuna taarifa kuwa mfanyabiashara huyo aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Trauma (AMI) iliyopo Msasani, amesafirishwa kupelekwa Afrika Kusini lakini hana taarifa zaidi kuhusiana na mwenendo wa tukio zima kwasababu wakati linatokea hakuwapo jijini Dar es Salaam.

Alisema hadi sasa polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo, hivyo hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa kutokana na unyama huo.

Hata hivyo chanzo cha habari toka ndani ya Jeshi la Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, kililidokeza  kuwa tukio hilo bado halijapangiwa askari kwa ajili ya upelelezi, hivyo taarifa kamili kuhusiana na mwenendo wa tukio lenyewe bado hazijakamilika.

Wiki iliyopita majira ya saa moja jioni, mfanyabiashara huyo alimwagiwa tindikali na mtu mmoja ambaye hakufahamika na mara baada ya kutenda tukio hilo, mhusika alikimbia huku mlinzi wa eneo hilo akijaribu kumkimbiza pasipo mafanikio baada ya kuteleza na kuanguka.

Hatua hiyo ilitoa mwanya kwa mtuhumiwa kutoroka eneo la tukio kwa kutumia usafiri aina ya pikipiki.

Hapo awali ilidaiwa kuwa Saad alikuwa anaweza kuzungumza japo amefungwa mashine sehemu ya pua kwa ajili ya kumsaidia kupumua.

Matukio ya watu kumwagiwa tindikali yameonekana kushamiri nchini katika siku za hivi karibuni.

Tukio la kumwagiwa tindikali mmiliki huyo wa Home Shopping Centre, limekuja ikiwa ni takribani wiki mbili tangu Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha, Said Juma Makamba naye ajeruhiwe vibaya usoni kwa kumwagiwa maji maji yanayosadikiwa kuwa ni tindikali majira ya usiku akiwa nyumbani kwake.(HABARI KWA HISANI YA MTANZANIA)

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...