Na Nathan Mtega,Mbinga
WAANDISHI wa habari mkoani Ruvuma
wametakiwa kuandika na kutangaza habari mbali mbali kwa kuzingatia maadili ya
kazi yao na kujiepusha na habari za uchochezi,ubaguzi na zinazochochea mifarakano
katika jamii kwa sababu jamii ina imani kubwa na wanahabari hasa wanaofanya
kazi yao kwa kuzingatia weledi na maadili ipasavyo.
Wito huo umetolewa na mwenyekiti wa
halmashauri ya wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma Allanus Ngai wakati akifunga kikao cha dharula cha
baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kilichofanyika bada ya uchaguzi wa
mwenyekiti na makamu mwenyekiti ambao awali uliahirishwa baada ya jina la
mwenyekiti huyo kuenguliwa katika mazingira ya kutatanisha na kusababisha
mtafaruku ndani ya halmashauri hiyo.
Alisema kuwa katika tukio hilo la kuenguliwa kwa baadhi ya majina ya
wagombea kwa ajili ya kundi moja kupanga safu yta uongozi ndani ya halmashauri
kwa manufaa yao waandishi wa habari mkoani Ruvuma walionyesha moyo wa uzalendo
kwa kutafuta ukweli na kuufanyia kazi kwa ajili ya maslahi ya walio wengi na
hawakuonyesha upendeleo wa aina yoyote katika kuitafuta haki hiyo ya wanyonge
ambayo hatimaye imepatikana.
Aidha alitoa pongezi kw waandishi wa habari huku akiwaasa kuepuka kutumiwa
na baadhi ya viongozi au kundi la watu ambalo lipo kwa ajili ya maslahi binafsi
kwa kuwatumia baadhi ya waandishi wa habari wasio waadilifu kujinufaisha na
kuendelea kuwadhulumu wanyonge walio wengi lakini katika tukio hilo la uchaguzi
wa viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga waandishi wa habari wameonyesha ukomavu wao na wanastahili pongzei.
Alisema kuwa waandishi wa habari waliandika na kutangaza ukweli kuhusu
mchakato mzima wa uchaguzi huo kwa kuwataja wahusika wa kupanga safu ya uongozi
ndani ya halmashauri hiyo kwa maslahi ya kundi fulani na kusababisha uchaguzi kusitishwa na hatimaye
ukweli huo umezaa matunda kwa jamii ya watu wa Mbinga.
Katika hatua nyingine mwenyekiti
huyo amewaagiza wakuu wa idara zote ndani ya halmashauri hiyo kutoa ushirikiano
mkubwa kwa waandishi wa habari na vyombo vya habari viweze kutangaza fursa za
maendeleo zilizopo ndani ya halmashauri hiyo na hatua zitachukuliwa dhidi ya
mkuu wa idara ambaye atathibitika kutoto ushirikiano kwa wanahabari kwa maslahi
au sababu binafsi.
No comments:
Post a Comment