Mke
wa Rais Mama Salma Kikwete akikaribishwa rasmi kwenye mkutano wa "High
Level Group" na Dr. Sheila Tlou, Mkurugenzi wa UNAIDS Regional Support
Team kwa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika katika siku ya pili ya
mkutano huo unaofanyika jijini Gaborone nchini Botswana tarehe 31 Julai
2013.
Mke
wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo Mama Salma
Kikwete akifunga rasmi mkutano wa High Level Group uliokuwa unafanyika
kwenye hoteli ya Lasmore nchini Botswana tarehe 31 Julai 2013.
Mke
wa Rais Mama Salma Kikwete akifanya mazungumzo na Profesa Alaphia
Wright, Mwakilishi wa UNESCO kwenye nchi za ukanda wa Kusini mwa Afrika
mwishoni mwa mkutano wa siku mbili wa High Level Group ulikuwa
ukifanyika jijini Gaborone nchini Botswana tarehe 31 Julai 2013.
Baadhi
ya wajumbe wa mkutano wakisoma jarida linalochapishwa na Taasisi ya
Wanawake na Maendeleo, WAMA, huku wakiendelea na mkutano.
Na Anna Nkinda- Gaborone, Botswana
1/8/2013 Jamii imetakiwa
kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha kuwa hakuna unyanyasaji wa
kijinsia kwa watoto wa kike pia inawalinda ili wasiingie katika
mazingira hatarishi yatakayowapelekea kupata kupata maambukizi ya
Virusi vya Ugonjwa wa Ukimwi (VVU) .
Wito huo umetolewa jana
na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na waandishi wa habari
mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa kamati maalum ya viongozi
wanaoshughulikia huduma na elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kutoka nchi
za Jumuia ya Afrika ya Mashariki (EAC) na Jumuia ya Ushirikiano wa
Maendeleo ya Kikanda kwa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika
katika Hoteli ya Lansmore Masa Square iliyopo mjini Gabarone nchini
Botswana.
Mama Kikwete ambaye pia
ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema huwa
anajisikia uchungu pale anaposikia kuwa mtoto wa kike amebakwa au
amefanyiwa ukatili wa kijinsia na kuiomba jamii nzima iweze kumsaidia na
kumkomboa mwanamke.
“Kama jamii yetu ya nchi
za kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika itaungana kwa pamoja na
kuamua kumsaidia mtoto wa kike itawezekana kwani hata kama watoto hawa
wakipata huduma bora ya afya bila ya kuwapatiwa elimu hakuna jambo la
maana watakalolifanya kwakuwa watakuwa na afya bora lakini watakosa
kujiamini kwani hawana elimu”, alisema Mama Kikwete.
Akiongelea kuhusu
Taasisi ya WAMA alisema kitaaluma yeye ni mwalimu na wakati anafundisha
aliona changamoto mbalimbali zinazowakabili watoto wa kike na pale
alipoanzisha taasisi hiyo aliamua kuwasaidia watoto wa kike ambao ni
yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi ambao wamekosa nafasi ya
kwenda shule ili nao waweze kusoma kama watoto wengine.
Mama Kikwete alisema, “
Tuna shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mfano ya WAMA-Nakayama ambayo
ina jumla ya wanafunzi 325 wa kidato cha kwanza hadi cha nne pia
Taasisi ya WAMA inawagharamia masomo wanafunzi wasichana 300 ambao
wanasoma shule mbalimbali za Sekondari katika mikoa yote ya Tanzania.
Alimalizia kwa kuiziomba
nchi wanachama wa EAC na SADC kutunga na kufuata sera na sheria
zitakazomlinda mtoto wa kike kwa kufanya hivyo ataepukana na unyanyasaji
wa kijinsia ikiwemo ubakwaji, udhalilishwaji, kutopewa huduma bora za
afya na elimu.
Mkutano huo wa siku
mbili uliandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupamba na Ukimwi
(UNAIDS) , UNFPA, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto
(UNICEF), Shirika la Chakula Duniani (WHO), Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia Sayansi na Utamaduni (UNESCO) lengo kuu likiwa ni
kuhakikisha kuwa vijana wote wanapata elimu kuhusiana na afya ya uzazi
na ujinsia na stadi za maisha jambo ambalo litawasaidia kufahamu zaidi
ugonjwa wa Ukimwi.SOURCE:IPSHA MEDIA
No comments:
Post a Comment