Leo ni Jumatano tarehe 28 Agosti 2013.
Miaka 52 iliyopita katika siku kama ya
leo, mwafaka na tarehe 28 Agosti 1963 Martin Luther King mwanaharakati
mkubwa wa kutetea haki za Wamarekani weusi nchini Marekani, alihutubia
umati mkubwa wa watu waliofanya mgomo wa kutaka wapewe haki ya kijamii
nchini humo. Luther King ambaye ni Mmarekani mweusi alihutubia umati huo
kwenye uwanja wa kumbukumbu wa Lincoln mjini Washington. Kwenye mkutano
huo, Martin Luther King alieleza ndoto yake ya kuwa huru Wamarekani
weusi.
Siku kama ya leo miaka 264 iliyopita
sawa na tarehe 28 Agosti 1749 alizaliwa Johann Wolfgang Von Goethe
malenga na mwandishi mkubwa wa Kijerumani. Von Goethe alisoma na
kujifunza mambo mbalimbali kama uchoraji na kadhalika katika mji
aliozaliwa wa Frankfurt nchini Ujerumani, huku akiendelea na masomo yake
ya taaluma ya sheria. Von Goethe ambaye anahesabiwa kuwa mmoja kati ya
waenezaji wa fasihi ya lugha ya Kifarsi, alivutiwa mno na fasihi ya
Kifarsi na hasa mashairi ya Hafidh, malenga na mshairi mashuhuri wa
Kiirani. Mwandishi huyo wa Kijerumani alikipenda sana Kitabu Kitakatifu
cha Qurani pamoja na dini ya Kiislamu. Johann Wolfgang Von Goethe
alifariki dunia mwaka 1832.
Na siku kama ya leo miaka 617 iliyopita
mtaalamu wa lugha na mwandishi mashuhuri wa zama hizo Majduddin Abu
Tahir Muhammad Yaaqub Firuzabadi aliaga dunia. Firuzabadi alikuwa pia
hodari katika taaluma za hadithi na tafsiri ya Qur'ani na ameandika
vitabu kadhaa katika taaluma hizo.
Hata hivyo kitabu mashuhuri zaidi cha
mwanazuoni huyo ni "al Qamus" ambacho ni miongoni mwa kamusi muhimu za
lugha ya Kiarabu. Vitabu vingine mashuhuri vya mwanazuoni huyo wa
Kiislamu ni "Sifrul Saada" na "Tanwirul Miqyas".
No comments:
Post a Comment