Watu
tisa wakiwemo wawili waliokuwa askari polisi wa kituo cha Osterbay
jijini Dar es Salaam wamepandishwa kizimbani katika mahakama ya hakimu
mkazi mkoa wa Pwani wakituhumiwa kwa makosa mawili ya kukutwa na nyara
za serikali na kushiriki katika kosa la kuhujumu uchumi kinyume cha
sheria.
Kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba moja ya mwaka 2013 inaunguruma
mbele ya hakimu mkazi nwandamizi mfawidhi wa mahakama hiyo Mh, Bahati
Ndeserua,ambapo wakili wa serikali Bi Cecilia Shelly akisoma hati ya
mashtaka mbele ya mahakama hiyo amewataja washtakiwa hao kuwa ni Koplo
Senga Idd Nyembo,Pc issa Mtama,wengine ni Prosper Mareto,Seif Kadro,Said
Kadro,wakazi wa panga la mwingireza vikumburu Kisarawe,Ramadhan
Athmani,Musa Ali dereva mkazi wa Kinondoni studio ambaye kazi yake ni
mgambo. Mahakama ikaambiwa kuwa,washtakiwa wote kwa pamoja wametenda
makosa hayo Julai 28 mwaka huu katika kituo cha ukaguzi cha kauzeni na
kijiji cha vikumburu Kisarawe mkoani Pwani,ambapo imedaiwa katika shtaka
la kwanza washtakiwa hao walikutwa na nyara za serikali ambazo ni
viapnde 70 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo 306 vyenye thaamni ya
shilingi milioni 850 na miatano mali ya serikali ya jamhuri ya muungano
wa Tanzania bila kuwa na kibali kutoka kwa mkurugenzi wa wanyama pori
nchini. Katika shtaka la pili wakili wa serikali akaiambia mahakama
kuwa,washtakiwa hao kwa pamoja walishiriki katika kosa la kuhujumu
uchumi kinyume na sheria na kwamba wakiwa katika kijiji cha Vikumburu
Kisarawe mkoani Pwani kwa nia ya kutenda uovu walikutwa na nyara za
serikali ambavyo ni vipande vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo 306.5
vyenye thamani ya shilingi milioni 850 mali ya serikali ya jamhuri ya
muungano wa Tanzania bila kuwa na kibali kutoka kwa mkurugenzi wa
wanyama pori nchini. Upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na
washtakiwa wote kwa pamoja hawakutakiwa kujibu lolote kisheria kwa kuwa
mahakama hiyo haina mamlaka kisheria ya kusikiliza kesi za aina hiyo na
wamerudishwa rumande hadi Agosti 14, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa
tena na upelelezi wa kesi mahakama imesema bado haujakamilika.
No comments:
Post a Comment