Saturday, August 24, 2013

RAIS KIKWETE AITAKA HALMASHAURI KUU YA CCM KUJADILI KWA KINA MAONI YA WANACHAMA JUU YA KATIBA


RAIS JAKAYA KIKWETE AKIFUNGUA MKUTANO WA CCM MJINI DODOMA
 Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) rais Jakaya Kikwete amewataka wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho kuhakikisha wanapitia na kujadili kwa kina maoni ya wanachama wao kuhusu mabadiliko ya katiba  ili kupata katiba itakayoliwezesha taifa kuendelea,kudumisha tunu zake za amani umoja na maelewano na kuondoa tofauti zilizoanza kujitokeza.
Rais Kikwete ametoa agizo hilo wakati akifungua mkutano wa wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Mjini Dodoma iliyokutana kama taasisi kujadili maoni ya wanachama wake kuhusu mabadiliko ya katiba ambapo rais Kikwete amesema katiba mpya ndio itakuwa dira ya maendeleo amani na ustawi wa taifa kwa kizazi cha sasa na kijacho.
 
Akimkaribisha rais Kikwete kufungua mkutano huo Katibu Mkuu wa CCM Abdurahmani Kinana amesema CCM imefanikiwa kukusanya  maoni ya wanachama zaidi ya milioni mbili na laki sita idadi ambayo mpaka sasa haijaweza kufikiwa na chama chochote cha siasa.
Kabla ya kufungua kikao hicho rais Kiwete alizindua Baraza la Ushauri la Wazee la CCM ambalo litakuwa na majukumu ya kutoa ushauri kwa chama na serikali katika mambo mbalimbali ambapo mwenyekiti wake ni rais mstaafu wa awamu ya pili Mhe Alhaji Ali Hasan Mwinyi  na katibu wake akiwa makamu mwenyekiti mstaafu wa CCM Mhe Pius Msekwa.

Katika hatua nyingine chama hicho kimetoa ufafanuzi kuhusu sakata la kufukuzwa kwa madiwani nane huko Bukoba ambapo katibu wa Itikadi na Uenezi Nape Nnauye amesema kamati kuu imeagiza Mweyekiti wa CCM na katibu wa Mkoa wa Kagera, mbunge wa Bukoba, meya wa Manispaa ya Bukoba, pamoja mwenyekiti wa CCM Bukoba mjini na katibu wake waitwe kujieleza mbele ya kamati kuu kuhusu sakata hilo na baadaye kamati kuu itatoa maamuzi kuhusu sakata hilo.Kamati kuu ya CCM na Halmashauri kuu ya chama hicho zinakutana mjini Dodoma kujadili mambo mbalimbali huku ajenda kuu katika vikao hivyo ikiwa ni kupitia maoni ya wanachama kuhusu mabadiliko ya katiba mpya na kisha maoni hayo kuwasilishwa tume ya mabadiliko ya katiba ambapo ccm inatoa maoni yake kama taasisi.
.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...