Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikifungua rasmi kituo cha Afya cha Sheia ya Chuini kilichopo Wilaya ya Magharibi. |
Uongozi wa Shehia zinazobahatika kupata
wawekezaji katika maeneo yao hapa nchini umetakiwa kujenga uhusiano mwema na
wawekezaji hao kwa lengo la kupata maendeleo ya haraka yatakayosaidia
kustawisha hali za wananachi wao.
Wito huo umetolewa na Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika hafla fupi ya kuzindua Kituo kipya cha
Afya katika Kijiji cha Chuini Wilaya ya Magharibi ikiwa ni mwanzoni mwa
maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka
1964 sawa na nusu Karne.
Balozi Seif alisema Uzoefu unaonyesha kuwa
wawekezaji wengi hapa nchini hupendelea kuchangia maendeleo ya wananchi lakini
mara nyingi hukatishwa tamaa kwa matumizi mabaya ya misaada wanayoitoa kunaofanywa
na baadhi ya Viongozi wa shehia kwa
kushirikiana na watendaji wabadhirifu wa Taasisi za Serikali na zile zisizokuwa
za Kiserikali.
Alionya kwamba tabia hiyo mbaya inarejesha
nyuma maendeleo ya Taifa na wananchi kwa jumla, hivyo hakuna budi kwa wenye
hulka hiyo kuachana nayo mara moja.
“ Mara nyingi na baadhi ya maeneo wawekezaji
wetu hukatishwa tamaa na udokozi wa baadhi ya wenzetu ambao hujisahau bila
ya kuzingatiwa kuwa wawekezaji hao ni
wageni wetu tuliyokwenda kuwatafuta ili waje kuwekeza nchini mwetu “.
Alifafanua Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza
wananchi na viongozi wa Shehia ya Chuini kwa kuwepuka matumizi mabaya ya
misaada ya wahisani jambo ambalo limesaidia kuwaletea maendeleo ya haraka.
Balozi
Seif alifahamisha kwamba wananchi wa Chuini wamefanikia
kuwa
na uadilifu mkubwa uliopelekea kulinda na kuheshimu michango
inayotolewa
na wahisani, wadau na washirika wa maendeleo ndani na
nje
ya Nchi.
Akizungumzia huduma za afya Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar ameiasa jamii kujenga utamaduni wa kuvitumia vituo vya afya
katika kujipatia huduma bora za afya pamoja na kupata taaluma ya kinga ya
maradhi tofauti.
Alisema tabia ya baadhi ya watu wakiumwa kufikiria
wamerogwa na kukimbilia kwa waganga wa kienyeji haina tija kwao na kwa kiasi kikubwa inaweza kuhatarisha maisha yao.
“ Tunapougua ni vyema tukakimbilia vituoni
ili kutibiwa. Tabia ya kukimbilia kwa waganga wa kienyeji kila mara, bila ya
sababu za msingi tuziache mara moja “. Alisisitiza Balozi Seif.
Aliwahakikishia Wananchi wa Shehia ya Chuini
kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa upande wake, itajitahidi kuona
dawa muhimu kwa ajili ya wananchi hao zinapatikana kituoni hapo pamoja na wafanyakazi
wa kutosha.
Kuhusu hali ya ukimwi hapa Nchini Balozi
Seif alisema maambukizi ya maradhi hayo imekuwa ikiongezeka kwa kasi badala ya
kupungua kama inavyoonekana sehemu nyengine duniani.
Alieleza kwamba Jitihada za Serikali za
kupambana na ukimwi hazitaweza kuleta mafanikio bila ya wananchi kushiriki
kikamilifu katika vita dhidi ya maambukizi na maradhi hayo ya Ukimwi.
Alitahadharisha kuwa ukimwi hauna tiba,
hivyo wananchi wajitahidi kujiepusha na vitendo vyote vinavyochangia kusambaa
kwa ukimwi hapa nchini, kama vile uzinifu, ngono zembe pamoja na utumiaji wa dawa za kulevya.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif katika kuunga mkono juhudi za wananchi hao wa Chuini ameahidi kuchangia
matofali elfu moja kwa ajili ya kuongeza nguvu za ujenzi wa jengo jipya la
Madaktyari wa Kituo hicho cha afya cha Shehia hiyo.
Katika risala yao wananchi hao wa shehia ya
Chuini iliyosomwa na katibu wa Kamati ya maendeleo wa shehia hiyo Bibi Narie
Mbaraka Kaite alisema Kituo hicho kilichogharimu jumla ya shilingi Milioni
28,000,000/- kitakuwa na huduma zote za msingi.
Bibi Narie alisema uongozi na wananachi wa
shehia hiyo hivi sasa wamejikita katika ujenzi wa nyumba ya familia mbili ya
daktari ikiwa katika hatua ya msingi ili jamii ya kijiji hicho ifikie hatua ya
kupata huduma za afya wakati wote.
Katibu huyo wa kamati ya maendeleo ya shehia
ya Chuini kwa niaba ya wananachi na viongozi wa shehia hiyo amewashukuru
wafadhili, wahisani na washirika wa maendeleo waliosaidia michango
iliyokamilisha ujenzi wa Kituo hicho cha afya.
Naye Mwakilishi wa wahisani na wafadhili wa mradi
wa ujenzi wa kituo hicho cha Afya Bwana Paul Jonson na Mkewe Bibi LNY wakitoa
salamu zao walisema Kituo hicho kitasaidia ukombozi wa kiafya kwa wananchi
walio wengi katika shehia hiyo.
Bwana Paul aliiomba Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kupitia Wizara inayohusika na masuala ya Afya kukipatria vifaa vya
kazi kituo hicho ili kiweze kutoa huduma bora na za kisasa.
Bibi Lny Paul akaisisitiza jamii ya
wazanzibari kujenga tabia ya kupenda kulinda na kutunza mazingira ili visiwa
vya Zanzibar viendelee kuwa na haiba nzuri.
Kituo cha Afya cha Chuini kitakuwa kikitoa
huduma zote za msingi ikiwemo mama wajawazito, watoto, maradhi ya kawaida,
ushauri nasaha pamoja namaabara.
No comments:
Post a Comment