Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na
Bunge,William Lukuvi, ameongoza mamia ya waombolezaji katika mazishi ya
aliyekuwa mwanamke wa kwanza nchini kusajiliwa na Bodi ya Wahandisi,
Grace Aikael Mbowe (57), ambaye ni dada wa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Wakati, Lukuvi akiongoza waombolezaji kwa niaba ya Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda, Mbunge wa Moshi Mjini (Chadema), Philemon
Ndesamburo alisimama wakati wa kutoa salamu za rambirambi kwa niaba ya
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Dk.Wilbrod
Slaa na kuwaonya waombolezaji na viongozi wa vyama vya siasa
waliojitokeza msibani kutothubutu kutumia msiba huo kama sehemu ya
kuhubiri siasa na badala yake waonyeshe upendo wao katika kuwatia nguvu
wafiwa
.
Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda, Lukuvi alisema serikali imepokea msiba huo kwa masikitiko
makubwa na kwamba ofisi yake inaungana na familia ya Freeman Mbowe
katika kipindi kigumu inachopita kwa sasa.
Grace alifariki katika ajali ya gari wiki iliyopita katika
eneo la Kabuku,Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga wakati akielekea jijini
Dar es Salaam.
Alikuwa mwanamke wa pili kusajiliwa na bodi ya wahandisi
nchini akiwa kama Ofisa mpimaji (Quantity Surveyer) baada ya kuhitimu
elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,kitengo ardhi (ARU).
Lukuvi na viongozi wengine wa serikali pamoja na Mwenyekiti
Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi na wabunge kadhaa wa Chadema,
waliongoza waombolezaji kumzika Grace katika makaburi ya familia, Kijiji
cha Nshara-Lambo,Tarafa ya Machame Wilaya ya Hai.
Katika mazishi hayo yaliyoongozwa na Askofu wa Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini, Dk. Martin
Shao, msemaji wa Chadema na mbunge wa jimbo la Moshi, Ndesamburo,
alisema Chadema imetoa rambirambi ya Sh.mil. 1,000,000.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa
Kilimanjaro, Idd Juma, alisema kifo cha Grace kimeacha pengo kubwa
katika familia ya Mbowe na kwamba hali hiyo isiwafanye watanzania
wakaacha kujenga undugu walionao na badala yake kiwafanye kuwa wamoja
zaidi.
No comments:
Post a Comment