|
Frank Nyalusi Mwenyekiti wa Chadema Iringa Mjini
|
|
Kama kawaida salamu za chama hicho za Peopleziii zilisika |
|
Mlemavu huyo
aliuliza swali katika mkutano huo akitaka kujua kati ya Samwel Sitta na
Rais jakaya Kikwete ni nani ana madaraka makubwa zaidi kuhusu mchakato
wa Katiba |
CHAMA
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Iringa Mjini, kimetangaza kufanya
maandamano ya amani LEO Jumatatu ikiwa ni hatua ya kuitikia wito wa
mwenyekiti wao, Freeman Mbowe wa kufanya maandamano hayo nchi nzima kushinikiza
kusitishwa kwa Bunge la Katiba.
Mwenyekiti
wa Chadema wa Iringa Mjin, Frank Nyalusi alitoa tangazo hilo jana katika
mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika katika mtaa wenye machinga wengi
maarufu kama Magari Mabovu, Kitanzani.
Katika
mkutano huo uliohudhuriwa na vijana kadhaa huku ukiwa umezungukwa na askari
Polisi kila kona, Nyalusi alisema “wapende wasipende, kesho tutafanya
maandamano, tunaomba Polisi washiriki kulinda usalama wetu, kwani maandamano
hayo yatakuwa ya amani.”
Alisema
maandamano hayo yanalenga kupeleka ujumbe wa kusitishwa kwa mchakato wa bunge
hilo kwa kuwa hauna maridhiano na fedha zitakazonusurika zitumike katika
shughuli zingine za kijamii.
“Hatuwezi
kupata Katiba kwa staili hiyo, tumemuomba Rais asitishe mchakato huo lakini
tumepuuzwa na sasa tunadhani ni zamu ya watanzania wote kupaza sauti zao ili
bunge hilo lisitishwe,” alisema.
Alipoulizwa
baadaye maandamano hayo yataanzia wapi, Nyalusi hakuwa tayari kutaja ni eneo
gani yataanzia kwa kile alichosema hawataki wapinzani wao wajue.
Kabla
ya kutangazwa kwa maandamano hayo ya kesho jumatatu, jeshi la Polisi
liliripotiwa na chama hicho kuwazuia kufanya maandamano kama hayo Jumamosi
iliyopita.
Badala
yake kwa mujibu wa Nyalusi, jeshi hilo liliwaruhusu kufanya mkutano wa hadhara
katika eneo hilo la Magari Mabovu.
Katika
mahojiano na gazeti hili, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa Ramadhani Mungi
alisema jeshi lake halijapokea maombi ya maandamano hayo kutoka katika chama
hicho.
Aliwataka wafuasi wa chama hicho kuzingatia
sheria, taratibu na kanuni wakati kikipanga na kufanya mambo yake.
Akitoa
ufafanuzi huo kwa njia ya simu, Mungi alisema; “nchi hii kama zilivyo nchi
nyingine inaendeshwa kwa sheria. Kwahiyo watu binafsi, serikali, vyama vya
siasa na wengine wote ni lazima wazingatie hilo.”
Alisema
mji wa Iringa upo shwari na kwamba jeshi hilo limejipanga kikamilifu
kukabiliana na hali yoyote ile itakayoonekana inataka kuhatarisha amani.
CREDIT:FRANCIS GODWIN