Rais Jakaya Kikwete, leo anaanza
ziara ya siku mbili mkoani Mbeya ambapo pia anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye
maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani maarufu kama Mei Mosi.
Maadhimisho hayo kitaifa mwaka huu
yanafanyika mkoani Mbeya.
Rais Kikwete, amewasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe
saa 4:30 asubuhi.
Awali mkuu wamkoa wa mbeya bw Abbas
Kandoro aliwataka wananchi hasa wakazi wa Jiji la Mbeya na vitongoji vyake,
kujitokeza kwa wingi kumlaki Rais Kikwete katika maeneo yote aliyotarajia kupita
akitokea Uwanja wa Ndege wa Songwe na pia kujitokeza kwa wingi kwenye sherehe
za Mei Mosi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) Mkoa wa Mbeya, Alinanuswe
Mwakapala, alisema maandalizi ya sherehe hizo yapo katika hatua nzuri na kuwa
anaamini kuwa kutokana na uwapo wa Rais Kikwete kama mgeni rasmi, yatafana
kuliko miaka ya nyuma.
Alisema sherehe hizo zinaandaliwa na
Tucta na kwa mwaka huu maandalizi yake yanaratibiwa na Chama cha Wafanyakazi wa
Meli na Bandari (Dowuta), huku kukiwa na kauli mbiu isemayo: ‘Katiba mpya
izingatie usawa na haki kwa tabaka la wafanyakazi’.
Mwakapa alitoa wito kwa waajiri wote
kuwaruhusu na kuhakikisha wafanyakazi wao wanashiriki kikamilifu katika sherehe
hiyo ili wafikishe madai na vilio vyao kwa waajiri.