Wednesday, October 22, 2014

MIAKA 10 TANGU KIFO CHA FREDY NDALA KASHEBA

ndala-kasheba_2255445 
LEO tunatimiza miaka kumi toka kifo cha mwanamuziki mahiri Freddy Supreme au maarufu kama Ndala Kasheba. Freddy alianza kufundishwa gitaa na baba yake wakati akiwa na umri wa miaka 12. Baba yake alijua kupiga gitaa japo hakufanya kazi ya uanamuziki, alikuwa akipiga gitaa nyumbani baada ya saa za kazi. Moja ya bendi maarufu ambazo zilimtambulisha sana Fredd ilikuwa Orchestra Fauvette, Freddy alieleza kuwa bendi ya Orchestra Fauvette ilianza tarehe 7 mwezi wa sita mwaka 1964 katika jiji la Lubumbashi huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Jina hilo Fauvette kwa kiswahili ni Chiriku, bendi ilikuwa na muimbaji ambaye waliamini alikuwa anaimba kama chiriku na hivyo kuipa bendi hiyo jina hilo. Vyombo vyao vya muziki walinunua Ujerumani kupitia duka la muziki la Dar es salaam Music House (duka lipo mpaka leo). Vyombo vilikuwa  vya aina ya Hofner, jina lililoheshimika sana kwa wanamuziki wakati huo.
IMG_2110
HILI NDILO KABURI LA FREDY NDALA KASHEBA LILIPO KINONDONI JIJINI DAR

Kati ya nyimbo ambazo zilipigwa katika kipindi hicho ni Camarade ya nzela, ambayo Freddy alieleza ni wimbo uliokuwa ukizungumzia rafiki wa kukutana nae barabarani au njiani, ambaye roho yake huwa kama sanduku la nguo, ambalo ndani yake huwezi kujua kuna nini. Pia ulipigwa wimbo Jacqueline ambao ulitungwa na mwenyewe Freddy ambao alieleza alikuwa alimtungia mpenzi wake aliyempenda Jacqueline. Wimbo mwingine uliopigwa katika kipindi hicho ni Nono na Kalemie, wimbo huu ulitunguiwa binti aliyeitwa Nono mkazi wa Kalemie ambaye alikuwa mpenzi mkubwa wa bendi ya Fauvette.
  Fauvette ilifika Dar na kuwa inapiga katika ukumbi wa White House Ubungo, lakini kwa miaka hiyo Ubungo ilikuwa mbali sana na mji, na kulikuwa na ajali nyingi zikiwapata wapenzi wa bendi katika usafiri wa kutoka kwenye muziki, hivyo bendi ikaamua kuhamia ukumbi wa Mikumi Tours ambapo walikuwa wakipiga Ijumaa, Jumamosi na Jumapili. Fauvette walikuwa na ndoto ya kuwa bendi bora Afrika. Hawakufikia huko lakini waliweza kuweka alama kubwa katika historia ya muziki wa Afrika mashariki na Kati
Kasheba aliweza kuimarisha jina lake zaidi alipolifanya maarufu gitaa la nyuzi kumi na mbili, mwenyewe akiliita nyuzi dazani, hasa alipoanza kulipiga kwa mtindo wa Dukuduku akiwa Safari Sound Orchestra. Pamoja na bendi hizo Kasheba pia alipitia Safari Nkoy, Zaita Muzika, Kasheba group, pia alipita Maquis, na kwa wiki chache alipitia Tancut Almasi.

Kasheba alifariki 22 Oktoba 2004 akiwa na miaka 58.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...